SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC) limeanza rasmi utekelezaji wa mradi wa ubia na kampuni ya Mikoani Traders, hatua inayotarajiwa kuleta mageuzi makubwa katika maendeleo ya makazi na biashara mkoani humo.
Kwa sasa, mradi upo katika hatua za awali za msingi, hatua muhimu inayoweka msingi imara wa ujenzi wa jengo la kisasa litakalokuwa kiungo cha biashara na makazi bora kwa wakazi wa eneo husika.
Kupitia ubia huu, NHC inalenga sio tu kujenga jengo la kisasa, bali pia kuchochea ukuaji wa miji, kuongeza ajira, pamoja na kuleta fursa mpya kwa wafanyabiashara wadogo, wa kati na wakubwa.
Akizungumza kuhusu maendeleo hayo, mmoja wa wawakilishi wa NHC alisema: “Tunayo furaha kuona mradi huu wa ubia ukianza kusimama rasmi. Ni hatua ya mwanzo lakini yenye matarajio makubwa kwa wananchi, kwani jengo hili litakuwa kitovu cha biashara na huduma muhimu.”
Mradi huu unaakisi dira ya NHC ya kuendeleza miradi mikubwa mikoani kwa ushirikiano wa karibu na wadau wa maendeleo, kuhakikisha wananchi wanapata makazi bora na maeneo ya kisasa ya kibiashara, huku miji ikibadilika kwa sura mpya yenye mvuto na tija kiuchumi.
Kwa ujumla, mradi huu ni sehemu ya dhamira ya NHC ya kuhakikisha maendeleo hayabaki Dar es Salaam pekee, bali yanagusa pia mikoa yote nchini, yakilinda kauli mbiu yake ya “Maisha ni Nyumba.”