MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango amesema Tanzania inasisitiza umuhimu wa mifumo endelevu ya ufadhili ili kuhakikisha uthabiti wa kukabiliana na dharura za afya ya umma barani Afrika.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati akishiriki katika Mkutano wa Kamati ya Wakuu wa Nchi na Serikali wa Kituo cha Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa Afrika (CDC) uliyofanyika pembezoni mwa Kikao cha 80 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Jijini New York nchini Marekani.
Amesema Tanzania imedhamiria kuongeza ukusanyaji wa rasilimali za ndani, kuimarisha masuluhisho ya kibunifu ya ufadhili pamoja na kuunga mkono mipango ya kikanda ambayo inapunguza utegemezi wa misaada kutoka nje, na hivyo kuhakikisha kuwa vipaumbele vya afya vya Afrika vinashughulikiwa na serikali za Afrika.
Aidha, Makamu wa Rais amesema uzalishaji wa ndani wa vifaa vya uchunguzi, matibabu, na bidhaa nyingine muhimu za matibabu ni muhimu katika kujitegemea kweye sekta ya afya.
Amesema Tanzania inahimiza uwekezaji katika viwanda vya ndani, mamlaka ya udhibiti ya pamoja barani kote, na ubia wa uhawilishaji wa teknolojia ili kuimarisha uwezo wa Afrika wa kukabiliana na changamoto za kiafya za sasa na zijazo.