Mbio za Mwenge zazindua mradi wa maji wa zaidi ya Bilioni

0

MBIO za Mwenge wa Uhuru zimezindua rasmi mradi wa maji wa Mkigo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma.

Mradi umetekelezwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kwa fedha kutoka Mfuko wa Taifa wa Maji kwa kushirikiana na Mpango wa Malipo kwa Matokeo (PforR).

Mradi umegharimu zaidi ya Shilingi Bilioni 1.9 na unatarajiwa kuwanufaisha wananchi zaidi ya elfu 14 katika kijiji cha Mkigo na vijiji jirani.

Lengo kuu ni kuhakikisha upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama, jambo linaloendana na dira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kumtua mama ndoo kichwani.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ismail Ali Ussi, katika uzinduzi aliipongeza RUWASA kwa usimamizi na utekelezaji bora wa mradi huo.

Alisisitiza kuwa mradi wa Mkigo ni kielelezo cha dhahiri cha jitihada za Serikali kuondoa kero ya maji vijijini na kusogeza huduma muhimu karibu na wananchi.

“Miradi ya aina hii inaleta suluhisho la kudumu kwa wananchi na ni matunda ya mshikamano kati ya Serikali na wadau katika kuhakikisha huduma za kijamii zinawafikia Watanzania wote bila ubaguzi,” Ussi amesema.

Kwa upande wake, Meneja wa RUWASA Mkoa wa Kigoma, Mhandisi Mathius Mwenda, amesema RUWASA itaendelea kuhakikisha miradi ya maji inatekelezwa kwa wakati na kwa viwango bora vinavyokidhi mahitaji ya wananchi.

“Tuna dhamira ya dhati kuhakikisha kila kijiji Kigoma kinapata huduma ya majisafi na salama. RUWASA itaendelea kusimamia miradi yote kwa ufanisi ili kufikia lengo la Serikali la kufikisha maji vijijini kwa kiwango cha zaidi ya asilimia 85 ifikapo mwaka 2025,” Mhandisi Mwenda amesisitiza.

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa Vijana na Ajira kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Suleiman Mvunye, ambaye pia ni mzaliwa wa kijiji cha Kalinzi, ametoa ushuhuda wa maisha ya kabla ya mradi akieleza changamoto walizokuwa wakipitia.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here