DKT. Habiba Hassan Omar, Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, ameongoza ujumbe wa Tanzania kwenye mjadala wa Mkakati wa Posta wa Dunia wa Dubai kwa kipindi cha 2026-2029.
Mkakati huo utakaokuwa wa miaka minne umejikita katika kujadili mwelekeo wa Posta katika mazingira ya sasa ya mabadiliko ya sekta ya Posta ambayo yanachagizwa na mabadiliko ya teknolojia na vionjo vya wateja.
Katika mijadala iliyoendelea jijini hapa inazingatiwa kuwa mtandao wa posta ndio muundombinu mkubwa zaidi wa usafirishaji duniani, ukiunganisha biashara na mabilioni ya watu, lakini inakumbushwa kuwa leo hii sekta inapitia mabadiliko makubwa ya biashara ya mtandaoni, huduma za kidijitali, mbinu mpya za utoaji huduma hivyo kwa uzoefu wake ni lazima ijibadili ili kuwa na uendelevu katika kuhudumia jamii.
Mkutano Mkuu pamoja na mambo mengine ni jukwaa ambalo mkakati wa namna Mtandao huu wa Posta kimataifa unaundwa, pia unaruhusu majadiliano juu ya viwango vipya utoaji huduma za posta, utoaji wa huduma jumuishi za kifedha, utoaji huduma kidijitali, na usalama wa mitandao.
Kwa mwaka huu lengo mahususi ni kujenga ushirikiano na miundo ya namna kuwashirikisha watoa huduma binafsi na watoa huduma wateule jambo linalotazamwa kuwa linaweza kufikia na kukidhi matarajio ya wateja na kuwa na uendelevu wa sekta ya Posta.