Vifaa vya Bilioni 1 kuboresha Usimamizi wa Misitu

0

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, amesema vifaa vyenye thamani ya zaidi ya Shilingi Bilioni 1 vilivyokabidhiwa kwa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) vitasaidia kuongeza ufanisi katika kulinda misitu na kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano iliyofanyika kwenye ofisi za WWF (TCO) jijini Dar es Salaam, Dkt. Abbasi alisema msaada huo kutoka Umoja wa Ulaya kupitia Shirika la Uhifadhi wa Mazingira Duniani (WWF) unaonyesha mshikamano wa kimataifa katika kulinda rasilimali za misitu na mazingira.

“Nawapongeza Umoja wa Ulaya na wadau wote kwa mchango huu. Vifaa hivi vitachangia si tu katika kuimarisha mifumo ya usimamizi wa misitu, bali pia katika kusaidia sekta muhimu kama nishati, maji na mazingira, ambazo zote zinategemea misitu,” alisema.

Mradi wa kupunguza uharibifu wa misitu

Vifaa hivyo vimekabidhiwa kupitia mradi wa Integrated Approach to Sustainable Cooking Solution (IASCS) unaotekelezwa kuanzia mwaka 2023 hadi 2026 katika mikoa saba ya Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma, Mwanza, Tabora, Tanga na Pwani.

Mradi huo unalenga kupunguza uharibifu wa misitu kwa kukuza matumizi ya nishati safi ya kupikia mijini na kuboresha mifumo ya usimamizi wa misitu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Savinus Kessy, Kiongozi wa Programu ya Nishati na Mabadiliko ya Tabianchi – WWF, mradi huo unatekelezwa kwa bajeti ya Euro Milioni 2.5 na unahusisha wadau mbalimbali wakiwemo Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA), Mpingo Conservation & Development Initiative (MCDI) na Lawyers’ Environmental Action Team (LEAT).

Thamani na vifaa vilivyotolewa

Vifaa vilivyokabidhiwa kwa TFS ni pamoja na magari 4, pikipiki 10, boti ya mwendokasi 1, mashine za malipo (POS) 25, mifumo ya mawasiliano ya redio 2, kompyuta za mezani 5, jenereta 5, kamera 5, pamoja na samani na vifaa vingine vya ofisi. Thamani ya vifaa hivyo ni Euro 346,852.65 sawa na Shilingi Bilioni 1.01.

Ushuhuda wa viongozi

Kamishna wa Uhifadhi wa Misitu TFS, Prof. Dos Santos Silayo, alisema msaada huo utaongeza ufanisi wa watumishi wa TFS katika kulinda misitu na kutoa huduma za ugani kwa jamii zilizo jirani na hifadhi.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki, Daniel Pancras, alisema vifaa hivyo vitasaidia kuimarisha usimamizi wa misitu ya jamii na kuongeza mchango wake katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Mkurugenzi Mkazi wa WWF Tanzania, Dkt. Amani Ngusaro, alisema msaada huo ni uthibitisho wa dhamira ya washirika wa maendeleo kuunga mkono juhudi za serikali katika uhifadhi wa misitu na kuboresha maisha ya wananchi.

Rai ya serikali

Serikali imetoa wito kwa watumishi wa TFS kuhakikisha vifaa hivyo vinatunzwa na kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa, ili kuimarisha usimamizi endelevu wa misitu na kuleta matokeo chanya kwa taifa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here