Mwenge wa Uhuru wazindua mradi wa maji wa Bilioni 3 Kagera

0

KIONGOZI wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ismail Ally Ussi, amezindua mradi wa upanuzi wa mtandao wa majisafi awamu ya pili wenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 3.15.

Mradi huu unaotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Bukoba (BUWASA).

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi, Ussi ameipongeza BUWASA kwa utekelezaji wa mradi huo na kuwataka wananchi kuulinda, akisisitiza kuwa mradi huo umeleta nafuu kubwa katika maisha ya wananchi hususan wanawake kwa kuwahakikishia huduma ya maji karibu na makazi yao.

“Mradi huu umemsaidia mama kumtua ndoo kichwani na sasa wananchi wanapaswa kuulinda ili uwe endelevu na kuwahudumia vizazi vya sasa na vijavyo,” Ussi amesema.

Kwa upande wake, Meneja wa BUWASA, Mhandisi Evodius Beyanga, alisema kukamilika kwa mradi huo kumeongeza upatikanaji wa maji kutoka asilimia 92 hadi 96, hatua inayodhihirisha dhamira ya Serikali katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma endelevu ya majisafi na salama.

Aidha, Beyanga aliongeza kuwa mradi huo unatarajiwa kuwahudumia wakazi wapatao 18,000 katika kata za Buhembe, Kahororo, Nshambya, Nyanga, baadhi ya maeneo ya Kata ya Kashai pamoja na Kata ya Nyakato.

Mradi huu ni sehemu ya jitihada za Serikali kupitia Sekta ya Maji kuhakikisha ifikapo mwaka 2030 wananchi wote wanapata majisafi na salama kwa mujibu wa malengo ya maendeleo endelevu (SDGs).

Kaulimbiu ya Mwenge wa Uhuru mwaka huu ni: “Jitokeze Kushiriki Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 kwa Amani na Utulivu.”

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here