Zaidi ya vijiji 136 kufikiwa na elimu ya utunzaji Mto Mara

0

ZAIDI ya vijiji 136 vinavyozunguka Bonde la Mto Mara vinatarajiwa kufikiwa na elimu ya utunzaji wa mto huo katika maadhimisho ya Siku ya Mto Mara yanayotarajiwa kuanza Septemba 12 hadi 15 wilayani Butiama mkoa wa Mara.

Mkuu wa Mkoa wa Mara Evans Alfred Mtambi amesema katika mkutano na vyombo vya habari.

Amesema elimu hiyo itasaidia kuulinda na kuuendeleza mto Mara ambao unachangia kwa kiasi kikubwa kuifanya hifadhi ya Taifa ya Serengeti kuwa moja ya Maajabu saba ya Dunia kutokana na uhamaji wa Wanyama kutoka Tanzania kwenda Kenya na kurudi Tanzania.

Mtambi amewaomba wananchi wa Mkoa wa Mara na maeneo jirani kujitokeza kwa wingi katika shughuli mbalimbali zitakazofanyika kwa kipindi hicho huku akisisitiza kuchangamkia fursa zitakazotokana na tukio hilo.

Amesema shughuli nyingine zitakazofanyika katika maadhimisho hayo ambayo huitimishwa kila Septemba 15, kipindi ambacho Nyumbu huvuka mto kuwa ni pamoja na upandaji wa miti zaidi ya 8,000, katika eneo linalopakana na mto, Kusimika vigingi (beacon) 50 kubainisha mipaka ya bonde na Kijiji cha Kirumi, Kongamano la Kimataifa la Kisayansi la Maji (International Maji Scientific Conference) ambalo huandaliwa na Wizara ya Maji, Chuo cha Maji, pia maonesho ya shughuli mbalimbali ikiwemo teknolojia za uhifadhi na ujasiliamali wa bidhaa.

Maadhimisho ya 14 ya Siku ya Mto Mara kwa mwaka 2025 yanaandaliwa kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Maji na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara kuanzia tarehe 12-15 Septemba katika uwanja wa Mwenge wilayani Butiama yakiwa na kauli mbiu isemayo ‘Hifadhi Mto Mara; Linda Uhai.’

Bonde hili lipo chini ya Wzara ya Maji kupitia Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria ambayo imekuwa na mikakati mbalimbali kuhakikisha maeneo yote yanayonufaikaa na mto huo hayaathiriki.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here