Kiboko msumbufu adhibitiwa Mto Ruvu

0

MAAFISA Wanyamapori wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha wakiongozwa na Afisa Wanyamapori wa Wilaya, Leonard Haule, wamefanikiwa kumdhibiti kiboko aliyekuwa akisumbua wananchi wa vitongoji vya Kisabi, Ruvu Dosa na Kidogozera vilivyoko kandokando ya Mto Ruvu.

Kiboko huyo alikuwa akitoka majini na kuingia kwenye makazi ya wananchi, kula mazao yao na kuhatarisha usalama wa wakazi pamoja na mifugo yao.

Akizungumza baada ya zoezi hilo, Haule alisema katika kipindi cha miezi mitatu pekee wamefanikiwa kudhibiti viboko wasumbufu watatu, hatua ambayo imeongeza usalama kwa wakazi wa maeneo hayo.

“Wananchi wanatakiwa waendelee na shughuli zao za kila siku bila hofu kwa kuwa sisi tupo kazini kuhakikisha wanalindwa dhidi ya wanyama wakali,” alisema.

Aidha, baada ya kumdhibiti kiboko huyo, nyama yake ilipimwa na daktari wa wanyama kisha kugawiwa kwa wananchi kwa ajili ya kitoweo.

Pamoja na hilo, maafisa wanyamapori walitumia fursa hiyo kutoa elimu ya kujikinga na wanyama wakali na waharibifu, ikiwemo kuepuka kulima karibu na mto chini ya mita 60 na kwenda kwa makundi wanapotekeleza shughuli kama kuteka maji ili kuepuka mashambulizi ya mamba. Haule alisisitiza kuwa elimu hiyo ni endelevu na itaendelea kutolewa mara kwa mara.

Wananchi wa vitongoji husika waliishukuru serikali kwa hatua ya mara kwa mara kupeleka maafisa wanyamapori katika maeneo yao na kwa elimu inayotolewa kuhusu namna bora ya kujiepusha na mashambulizi ya wanyama wakali kama viboko na mamba.

Pia, walihimizwa kutoa taarifa mapema pindi wanyama hao wanapoonekana ili wadhibitiwe haraka na kuepusha madhara.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here