HALMASHAURI ya Wilaya ya Kibaha kupitia Idara ya Fedha imeendesha mafunzo ya Mfumo wa Usimamizi wa Fedha ulioboreshwa (Facility Financial Accounting and Reporting System – FFARS), yaliyofanyika katika ukumbi mkuu wa Halmashauri.
Akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji, Mweka Hazina wa Halmashauri, Zainabu Mzindikaya, aliwataka washiriki kufuatilia kwa umakini ili kuongeza tija na ufanisi katika usimamizi na ulipaji wa fedha za umma.
Pia, aliwakumbusha kuyatumia mafunzo hayo ipasavyo ili kuepusha hoja za ukaguzi zisizo na msingi.
Kwa upande wake, mkufunzi wa mafunzo hayo, Gerald M. Nalugendo, aliwasisitiza washiriki kufuata taratibu zote za msingi za mfumo wa FFARS ili kuepuka makosa na kuhakikisha malipo yote yanafanyika kupitia mfumo rasmi.
Aidha, Afisa kutoka Benki ya NMB, Joel Mwanjegele, alitoa elimu ya Internet Banking kwa washiriki.
Alieleza kuwa, maboresho ya FFARS yanaenda sambamba na matumizi ya Internet Banking, ambayo yanaondoa usumbufu wa kubeba hundi kwa watumishi waliokasimiwa majukumu ya usimamizi wa fedha, na badala yake kurahisisha malipo kwa njia ya Kielektroniki.
Mafunzo haya ya siku mbili yamehudhuriwa na watumishi wa umma kutoka idara mbalimbali ikiwemo Elimu, Afya, Kilimo pamoja na Utawala, wakiwemo Maafisa Watendaji wa Kata na Vijiji.