📌 Asema Kuna Maisha baada ya Uchaguzi
📌 Amwakilisha Rais Samia, miaka 40 Kanisa Anglikana Dayosisi ya Kagera
📌 Rais Samia achangia Shilingi Milioni 50 Ujenzi wa Kanisa Dayosisi ya Kagera
📌 Anglikana Waishukuru Serikali, washirika wa maendeleo
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amewataka Watanzania kuwapima wagombea wa nafasi mbalimbali katika Uchaguzi Mkuu ujao na kuchagua kwa haki ifikapo Oktoba 29, 2025 (mwaka huu) na katu wasikubali Uchaguzi uwagawe.
Dkt. Biteko amesema hayo Agosti 12, 2025 wakati akimwakilisha Mheshimiwa Rais katika Kilele cha Maadhimisho ya Miaka 40 ya Kuzaliwa kwa Dayosisi ya Kagera iliyofanyika katika Viwanja vya Kanisa Kuu Yohana Mbatizaji – Murgwanza, Ngara.
Alisema, watanzania wanayo haki ya kuwapima wagombea kwa matendo yao na hatimaye kutenda haki kwa kufanya uchaguzi wao kwa njia ya demokrasia huku akisisitiza umuhimu wa kuzingatia kampeni za kistaarabu na kujiepusha na vitendo vya uvunjifu wa maadili.
Akiwasilisha salamu za Rais, Dkt. Biteko alisema, Dkt. Samia anatambua na kuheshimu mchango wa taasisi za dini na mchango wake katika maendeleo ya Taifa. “ Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ni mdau wa kujenga na kila mnachokifanya kinalenga katika maendeleo ya watu hivyo anaunga mkono jitihada za maendeleo ya wananchi,”
Katika kufanikisha azma yake, Rais Dkt. Samia amechangia Shilingi Milioni Hamsini (50,000,000/=) katika harambee ya ujenzi wa Kanisa jipya la Anglikana Dayosisi ya Kagera.
Dkt. Biteko amesisitiza umuhimu wa kila mtu kuwa kisababishi cha furaha kwa mwenzake ili kuwa na maisha ya ya furaha.
Awali, Askofu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dayosisi ya Kagera, Darlington Misango Bendankeha ameishukuru Serikali kwa ushirikiano mkubwa unaopatikana katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Askofu Bendankeha amesisitiza kuwa, Serikali katika ngazi zote inatoa ushirikiano na hivyo kufanikisha utekelezaji wa miradi ya Afya, Elimu kwa maendeleo ya jamii.
Ameiomba Serikali kufanikisha ujenzi wa Barabara inayounganisha taasisi mbalimbali za utoaji wa huduma yenye urefu wa mita 900, Gari la wagonjwa pamoja na mchango wa ujenzi Kanisa ambalo ujenzi wake unaendelea kwa gharama ya Shilingi Bilioni 1.18
Kufuatia maombi hayo, Dkt. Biteko amemwelekeza Mkuu wa Mkoa, Mkuu Wilaya na Wakala wa Barabara mijini na vijijini (TARURA) kufanikisha ujenzi wa Kipande hicho huku akitoa ahadi ya gari la wagonjwa katika Hospitali ya Murgwanza baada ya kuwasiliana na Waziri wa Afya, Jenista Mhagama.
Akizungumzia uchaguzi Mkuu ujao, Askofu Bendankeha amewahimiza wananchi kushiriki kikamilifu na kuwachagua viongozi wao katika uchaguzi Mkuu ujao ili kuchochea maendeleo “ Tujiandae kushiriki uchaguzi Mkuu ujao, kura yetu ndiyo nguvu ya mabadiliko.”
Naye Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatuma Mwassa amelipongeza Kanisa la Anglikana Tanzania kwa huduma mbalimbali za maenseleo zinazotolewa kwa jamii.