WMA wafanya ukaguzi wa kushtukiza soko kuu Kibaigwa, watoa onyo

0

WAKATI Maonesho ya Kimataifa ya Wakulima (NaneNane) 2025 yakiendelea, Wakala wa Vipimo (WMA) wamefanya ukaguzi wa kushtukiza kwenye soko kuu la Kimataifa la mazao Kibaigwa, jijini Dodoma.

Akizungumza mara baada ya ukaguzi huo, uliofanyika leo, Agosti 5, 2025 Afisa Mwandamizi wa Vipimo Said Ibrahim alisema, wamekuta mizani nyingi zinapima vizuri, ingawa kuna chache ambazo zinahitaji marekebisho ambayo wameyafanya na zipo tayari kwa matumizi.

“Tumepitia mizani zote, zipo salama na tayari kwa kupima mazao ya wakulima,” alisema Afisa huyo, huku akitoa wito kwa wafanyabiashara ambao wanachezea mizani waache mchezo huo na kuwataka watumie mizani iliyohakikiwa.

Alisema, wakala wa vipimo watachukua hatua kali za kisheria kwa wafanyabiashara ambao wanafanya vitendo hivyo na kusisitiza kwamba, zoezi hilo ni endelevu.

Wakala wa Vipimo, ni miongoni mwa taasisi zinazoshiriki Maonesho ya Kilimo, maarufu kama Nanenane, yanayofanyika kwenye uwanja wa Nzuguni, Dodoma.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here