Mfumo wa ufundishaji mubashara mbioni kutumika nchi nzima

0

Na James Mwanamyoto

SERIKALI imeeleza azma ya kuhakikisha Mfumo wa Ufundishaji Mubashara (live teaching) unaanza kutumika nchi nzima ili kumuwezesha mwalimu kutoka katika kituo kimoja kufundisha wanafunzi wengi kwa wakati mmoja wakiwa katika mikoa tofauti.

Azma hiyo ya Serikali imeelezwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mohamed Mchengerwa, alipofanya ziara ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa walimu na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kibaha ambayo ina kituo (smart class) cha ufundishaji mubashara (live teaching).

Waziri Mchengerwa alisema, anatambua kuwa Kibaha Sekondari ni moja ya kituo kinachotegemewa kwa ajili ya ufundishaji mubashara kwani mwalimu anaweza kufundisha akiwa Kibaha Sekondari na wanafunzi nchi nzima wakaudhuria kipindi chake.

“Kibaha Sekondari ni lazima muendelee kutumia Mfumo wa Ufundishaji Mubashara kwani niliuzindua mwenyewe jijini Dodoma kwa kuiunganisha Kibaha Sekondari na Dodoma Sekondari na tulijionea namna mfumo unavyofanya kazi na sasa tunataka uende nchi nzima,” Mchengerwa alisisitiza.

Sanjari na hiyo, Mchengerwa amempongeza Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha Dkt. Rogers Shemwelekwa kwa kuhimiza matumizi ya Mfumo wa Ufundishaji Mubashara katika Shule ya Sekondari Kibaha na kumtaka aendelee kuiwezesha shule hiyo kuwa kituo cha mfano cha ufundishaji mubashara nchini, kwani wakati akiwa Shirika la Elimu Kibaha aliwezesha mfumo huo kufanya kazi.

Waziri Mchengerwa amefafanua kuwa, iwapo miundombinu ya elimu itaendelea kuboreshwa katika Shule ya Sekondari Kibaha, hapo baadae kuna uwezekano Serikali ikafikiria kujenga chuo kikuu katika eneo hilo hilo ambalo shule hiyo ipo ili kutimiza lengo la Rais Samia la kuhakikisha kila mtanzania anapata elimu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here