Prof. Nagu asisitiza usimamizi wa mapato sekta ya afya msingi

0

NAIBU Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI anayeshughulikia Afya, Prof. Tumaini Nagu, amezisisitiza timu za usimamizi wa shughuli za Afya za Halmashauri (CHMT) kuongeza kasi ya usimamizi wa ukusanyaji wa mapato katika maeneo ya kutolea huduma za afya nchini.

Maelekezo hayo ameyatoa Julai 23, 2025 katika Kituo cha Afya Malezi wilaya ya Handeni mkoa wa Tanga katika ziara ya usimamizi shirikishi akiwa ameambatana na wataalamu wa Afya kutoka Ofisi ya Rais – TAMISEMI ambapo alisema, ukusanyaji wa mapato unatakiwa kufanyika kwa ufanisi na kufuata miongozo iliyowekwa.

“Miundombinu hii imetumia gharama hivyo tunatakiwa kuilinda na kuhakikisha uendelevu wa huduma unaendana na ugharamiaji wa huduma.” alisema.

Prof. Nagu amesisitiza kuwa fedha zote zitakazokusanywa zinapaswa kuingizwa kwenye akaunti maalum za kituo ili zitumike kuboresha huduma za afya na kuwapatia motisha wafanyakazi.

Aidha, ameongeza kuwa ni muhimu kuachana na matumizi ya fedha taslimu katika vituo vya kutolea huduma za afya kwaajili ya usalama wa fedha hizo.

“Tuhakikishe hatuchukui fedha taslimu bali tumieni ‘Control number’ ili fedha zote zinazopatikana zihakikishwe kwenye mifumo yetu,” alisisitiza Prof. Nagu.

Pia, ametoa wito kwa wakurugenzi wa halmashauri nchini kutuma wataalamu katika maeneo ya kutolea huduma ili kufuatilia matumizi ya fedha kwa karibu.

Katika hatua nyingine Prof. Nagu amewataka wataalamu wa afya kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kujiunga na bima ya afya.

Prof. Nagu yupo mkoani Tanga kwaajili ya ziara ya usimamizi shirikishi akiwa ambatana na wataalamu wa Afya kutoka Ofisi ya Rais – TAMISEMI lengo likiwa ni kuendelea kuhamasisha ubora wa huduma za Afya kwa wananchi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here