Na Aron Msigwa, MAELEZO
SERIKALI imeupatia Mkoa wa Mara kiasi cha Shilingi Bilioni 43.41 katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ili kujenga miundombinu ya afya na kusogeza huduma za afya karibu na wananchi.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Idara ya Habari – MAELEZO kupitia programu ya Tumewafikia, Tumewasikia Julai 1,2025 Jijini Dodoma, Mkuu wa Mkoa wa Mara Kanali Evans Alfred Mtambi amesema fedha hizo zimetolewa kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa hospitali mpya nane za Halamashauri ambazo tayari zimeanza kutoa huduma.
“Mkoa umepokea Shillingi Bilioni 43.41 kuanzia 2021/2022 hadi 2024/2025 kwa ajili ya utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu ya sekta ya afya, Kuongezeka kwa vituo vya kutolea huduma kumepunguza umbali wa wananchi kupata huduma za afya kutoka wastani wa Kilomita 15 mwaka 2020 hadi kilomita 5 mwaka 2025” alisema Kanali Mtambi.
Ameongeza kuwa fedha hizo pia zimetumika katika ukarabati na upanuzi wa hospitali ya Manispaa ya Musoma ili iweze kutoa huduma bora kwa wananchi ambapo pia vituo vya Afya 14 na zahanati 70 zimejengwa na kuanza kutoa huduma kwa wananchi ndani ya kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Samia.
Aidha, ameeleza kuwa Serikali inaendelea na ujenzi wa vituo vya Afya vipya vinne vya Mwibagi, Wegero na Kiabakari, Wilaya ya Butiama na Kuruya, Wilaya ya Rorya.
Mafanikio mengine yaliyopatikana katika hiyo ni kuongezeka kwa vituo vya kutolea huduma za Afya kutoka vituo 321 mwaka 2020 hadi 421 mwaka 2025, Kliniki zinazotoa huduma zimeongezeka kutoka 4 hadi 11, zahanati kutoka 263 hadi 333.
Kanali Mtambi ameongeza kuwa idadi ya vituo vya Afya ndani ya mkoa huo imeongezeka kutoka 42 hadi 56, hospitali kutoka 11 hadi 20, hospitali za Halmashauri kutoka tatu hadi 11, nyumba za watumishi kutoka nyumba 221 mwaka 2020 hadi 286 mwaka 2025.