Sekta ya hifadhi ya mazingira yapewa kipaumbele Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050

0

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ameitaja sekta ya hifadhi ya mazingira kuwa ni miongoni mwa maeneo ya kipaumbele katika Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2050.

Hayo yamejiri wakati wa hafla ya uzinduzi wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 iliyofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete (JKCC) Jijini Dodoma Julai 17, 2025.

Akizungumza katika hafla hiyo Dkt. Samia alisema, nchi lazima iendelee kujipambanua na kuwa sehemu ya juhudi za kimataifa za kulinda mazingira ambapo Nguzo ya Tatu ya Dira hiyo ni Uhifadhi wa Mazingira na Ustahimilivu wa Mabadiliko ya Tabianchi.

Dkt. Samia alisema, hatuna budi kuweka mikakati ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi hapa nchini kwani yanaendelea kuathiri sera za kitaifa na kimataifa, ikiwemo suala la uzalishaji na usalama wa chakula.

Aliongeza kuwa, Dira 2050 imeweka bayana malengo na shabaha za maendeleo ili kuijenga ‘Tanzania Tunayoitaka’ ikiwemo kujenga taifa linalohifadhi na kutumia rasilimali za asili kwa ufanisi, uendelevu na tija na linalostahimili mabadiliko ya tabianchi.

Maeneo ya kipaumbele katika Dira 2050 ni Uhifadhi wa Bioanuai matarajio yakiwa ni kuwa miongoni mwa nchi mahiri katika uhifadhi wa bioanuai, yenye mifumo bora ya ikolojia, ambapo aina mbalimbali za viumbe hai zinastawi katika makazi yao ya asili.

Pia, Taifa kinara kwa matumizi endelevu ya bioanuai kwa manufaa ya ustawi wa jamii na maendeleo ya kiuchumi kwa kizazi cha sasa na kijacho na linalokokotoa vyema thamani ya rasilimali za bioanuai na maliasili za nchi ili zitumike kikamilifu kuchangia katika pato la taifa na maendeleo ya jamii.

Kipaumbele kingine ni Uhifadhi wa Ardhioevu na Vyanzo vya Maji matarajio yakiwa ni ardhioevu bora zinazochangia ustawi wa watu, kukuza uchumi na kutoa huduma muhimu za kiikolojia, Taifa lenye uhakika na usalama wa maji kwa ajili ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi na linalodumisha na kuendeleza uhifadhi wa ikolojia na mfumo imara na shirikishi wa usimamizi wa ardhioevu, maji na rasilimali nyinginezo.

Dira 2050 imeanisha Udhibiti wa Uchafuzi wa Mazingira kuwa ni kipaumbele kingine ambapo ambapo matarajio ni Jamii yenye uelewa mkubwa wa athari za uchafuzi wa mazingira ili kuwa na mazingira salama na endelevu kwa wote, majiji na miji yenye miundombinu na usimamizi bora wa taka na ujenzi unaozingatia uhifadhi wa mazingira, Taifa kinara katika matumizi endelevu ya rasilimali na linalotumia taka na Taifa lenye mazingira stahimilivu linalosimamia vyema maliasili kwa maendeleo ya uchumi wa kijani.

Halikadhalika, Usimamizi Madhubuti wa Ardahi umetajwa katika Dira 2050 na matarajio ni Nchi iliyopangwa vizuri na kuweka wazi matumizi ya ardhi, yakiwemo ya makazi, kilimo, mifugo, viwanda na hifadhi, Usimamizi bora wa ardhi unaoongozwa na nguvu ya soko la ardhi, mali isiyohamishika na huduma, ili kuvutia uwekezaji unaotegemea ardhi.

Matarajio mengine ni Jamii yenye usawa ambapo kila mwananchi, hususan wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, wanapata fursa sawia za umiliki wa ardhi na Taifa ambalo mipaka imepimwa kwa usahihi, kuimarishwa kikamilifu na inayotambulika kimataifa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here