MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri kuongeza juhudi katika kutoa hamasa kwa wananchi ili kuzingatia kanuni za afya bora na kuchukua hatua madhubuti za kujikinga na magonjwa ya kuambukiza na yale yasiyo ya kuambukiza.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati akifungua Mkutano wa Mwaka wa Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri unaofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete mkoani Dodoma.
Alisema, ni vema elimu itakayotolewa izingatie ujenzi na matumizi ya vyoo bora, unawaji mikono kwa maji tiririka na sabuni nyakati zote muhimu ili kukabiliana na magonjwa ya kuambukiza, uondoshaji salama wa majitaka katika ngazi ya kaya na maeneo ya umma pamoja na kutibu maji ya kunywa kwa njia ya kuchemsha au kwa kuzingatia maelekezo ya wataalam.
Vilevile, Makamu wa Rais ametoa rai kwa Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri kuvitunza vifaa tiba ikiwemo mashine za kisasa za uchunguzi na matibabu pamoja na magari ya kubeba wagonjwa yaliyonunuliwa na Serikali ili viweze kutumika kwa muda mrefu na kutoa huduma kwa watu wengi zaidi.
Pia, amewasihi kuimarisha eneo la utunzaji wa kumbukumbu za matumizi ya dawa na vifaa tiba ili kuleta ufanisi katika utunzaji wa dawa na vifaa tiba na kuepuka upotevu.
Alisema, kutokuwepo na kumbukumbu sahihi za matumizi ya dawa na vifaa tiba hutatiza katika usambazaji wa dawa kutoka Bohari Kuu ya Dawa, na kutoa mwanya wa wizi na matumizi yasiyo sahihi.
Halikadhalika Makamu wa Rais amewaagiza Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri kulipa kipaumbele suala la utoaji wa elimu ya matumizi sahihi ya dawa ili kuisaidia jamii kutambua na kuepuka madhara ya matumizi holela ya dawa hususani dawa za maumivu na antibiotics ambazo zikitumiwa kiholela madhara yake ni makubwa. Pia amewataka kusimamia kwa ukaribu utekelezaji wa kiapo cha maadili katika kuwahakikishia wananchi huduma bora.
Aidha, ameziagiza Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha zinasimamia vema ukusanyaji wa mapato na kuhakikisha yanatumika kiadilifu ili kuboresha zaidi utoaji wa huduma wakati Serikali inapoelekea kutekeleza mpango wa Bima ya Afya kwa Wote.
Alisema, katika kuhakikisha utoaji wa huduma bora za afya, Serikali imeweka kipaumbele suala la rasilimali watu yenye weledi, ambapo imeajiri jumla ya watumishi wapya 25,936 wa kada mbalimbali za afya katika ngazi ya msingi.
Hatua hiyo, imesaidia kukabili upungufu wa watumishi na kuongeza uwiano kati ya watoa huduma na wagonjwa.
Aliongeza kwamba, Serikali itaendelea kutoa kipaumbele katika eneo hilo hususani kwenye kada za kimkakati, ili kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora na endelevu kwa wananchi.