‘Mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA 2025 ni ya kipekee’

0

OR-TAMISEMI, Iringa

YUSUF Singo, Mmoja wa waratibu wa Mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma Tanzania kwa Shule za Msingi na Sekondari (UMITASHUMTA & UMISSETA 2025) ameelezea kuwa michezo ya mwaka huu ni ya kipekee na ina utofauti.

Akizungumza katika mahojiano maalum na Jarida hili, Singo alisema upekee wa Mashindano hayo umeletwa na namna ambavyo mikoa imejiandaa kushindana na kuvunja rekondi mbalimbali ambazo zimekuwa zikiwekwa katika michezo tofauti.

“Kuna rekodi nyingi zimevunjwa, mfano kwenye riadha wapo vijana wawili kupitia mashindano haya wamechaguliwa kwenda kushiriki mashindani ya Kimataifa.”

Singo pia ameelezea uwepo wa waamuzi vijana ambao wamechezesha michezo ya Netiboli, Kikapu na Mpira wa mikono, kuwa ni mpango endelevu unaolenga kuibua waamuzi na wasimamizi mahiri wa michezo nchini katika siku zijazo.

“Tulifanya utafiti tukagundua kuwa kuna mapungufu katika baadhi ya maeneo ikiwepo waamuzi na tukaona tuje na mpango wa muda mrefu wa kuandaa vijana kuanzia ngazi ya chini watakaokuja kulitumikia Taifa kitaifa na kimataifa katika siku zijazo”

“Tumeanza na hawa wachache wastani wa 10, kwa michezo mitatu, wataongezeka kwenye mashindano yajayo, na sio waamuzi tu lakini pia tunawafundisha usimamizi wa michezo ikiwezekana siku zijazo wajisimamie wenyewe”

Kwa upande wa maandalizi, Singo amewapongeza viongozi mbalimbali wa mkoa wa Iringa kwa kuonesha ushirikiano mkubwa ambao umepelekea wanamichezo kufurahia mazingira ya kimichezo.

Mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA 2025, yameandaliwa na Ofisi ya Rais-TAMISEMI ikishirikiana na Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia pamoja na Wizara ya Elimu, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here