MKURUGENZI Mkuu wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) Dkt. Emmanuel Mkilia amezitaka taasisi za umma na binafsi nchini kusimamia mipango ya kupunguza vihatarishi katika ulinzi wa taarifa binafsi.
Dkt. Mkilia ameyasema hayo wakati akifungua mafunzo ya kupunguza vihatarishi katika ulinzi wa taarifa binafsi kwa wasimamizi wa vihatarishi wa taasisi za umma na binafsi yanayofanyika katika ukumbi wa mikutano wa hoteli ya Lush Garden iliyopo jijini Arusha.
“Kusudio la mafunzo haya si kuongeza maarifa tu kwenye kazi, bali ni hatua ya kujenga utamaduni mpya wa usalama wa taarifa binafsi zinazokusanywa na kuchakatwa na Taasisi zenu,” alisema Dkt. Mkilia.
“Natoa wito kwenu kasimamieni na kuanzisha mipango ya ndani ya kupunguza vihatarishi katika Ulinzi wa Taarifa Binafsi; fanyeni tathmini na kuboresha sera na mifumo yenu ya TEHAMA; na shirikianeni na Tume kwa ukaribu katika kutoa taarifa na kupata ushauri wa kitaalamu kuhusu Ulinzi wa Taarifa Binafsi,” alisema Dkt. Mkilia.
Wakati huo huo, Katibu Mtendaji wa Chuo cha Usimamizi wa Vihatarishi (IRMT) Christopher Njovu ametoa rai kwa taasisi za umma na binafsi kuzingatia kupata elimu hiyo na kuhakikisha maafisa wao wanakuwa wataalamu walioidhinishwa kusimamia vihatarishi.
“IRMT tunatoa mafunzo ya kutengeneza na kuthibitisha wataalamu wa usimamizi wa vihatarishi nchini Tanzania, hivyo nawasihi mje mpate mafunzo haya na vyeti vya kuwathibitisha kuwa ni wataalam wa eneo hili,” alisema Njovu.
Mafunzo hayo ya siku tatu ni moja ya njia ya kuhakikisha taasisi za umma na binafsi zinakuwa na utaratibu wa kutambua viashiria vya vihatarishi hivyo na kuchukua hatua stahiki kabla hatari haijatokea.