Rais Samia aweka jiwe la msingi mradi wa shule 103 za amali

0

Na John Mapepele, OR TAMISEMI

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt, Samia Suluhu Hassan leo ameweka Jiwe la Msingi katika Shule ya Sekondari ya Amali ya Mwamapalala kwa niaba ya mradi wa shule 103 zinazojengea kote nchini.

Hadi sasa tayari Serikali imetoa jumla ya Shilingi Bilioni 41.6 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya 26 za Sekondari za Amali za Mikoa.

Kati ya fedha hizo, Mkoa wa Simiyu kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Itilima ilipokea Shilingi Bilioni 1.6 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ya Amali ya Mkoa wa Simiyu.

Akiwahutubia wanachi waliokusanyika katika shule hiyo Rais alisema, lengo la ujenzi wa shule hizo ni kuwawezesha Wanafunzi kupata ujuzi wa ziada hasa katika fani za ufundi ili waweze kujiajiri baada ya kuhitimu elimu yao ya Sekondari.

“Mwelekeo wa Serikali ya Awamu ya Sita kwa sasa ni kukukuza elimu ya Amali ili vijana wetu wanaomaliza waweze kujiajiri,” alifafanua Rais.

Aliongeza, kutokana na wimbi kubwa la watoto wanaomaliza shule, Serikali peke yake haiwezi kuwaajiri wote hivyo watakaopitia katika shule hizi watakuwa na uwezo wa kujiajiri pia kuajiriwa na sekta binafsi.

Alisema, Serikali inatumia fedha nyingi kujenga shule hizo na amewataka wazazi wote nchini kuwapa fursa watoto ili wapate ujuzi katika shule hizi maalum.

Aidha, Rais alisema katika kipindi hiki Serikali yake kumekuwa na mabadiliko makubwa ya maendeleo katika wilaya ya Itilima na kutaka barabara za ndani ya Wilaya hiyo pamoja na taa za barabarani kuwekwa.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mohamed Mchengerwa akielezea utekelezaji wa mradi wa shule hizo kwa Rais alisema, mradi huo ni dhamira na ndoto za kuwapatia wanafunzi elimu ya ufundi ili waweze kujitegemea baada ya kumaliza masomo ya Sekondari.

“Mhe. Rais mara baada ya kuniteua kuwa waziri wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI uliniagiza nishirikiane na Waziri wa Elimu kusimamia utekelezaji wa mradi huu,” aliongeza Mchengerwa.

Aidha, Mchengerwa amezitaka Halmashauri zote zilizopitiwa na mradi huu kujenga uzio kwa mapato ya fedha za ndani ili kuimarisha ulinzi kwa wanafunzi.

Naye Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof.Adolf Mkenda amesema kwa kushirikiana na TAMISEMI wameweza kutekeleza mradi huu kwa mafanikio.

Aidha, alisema mfumo huu wa sasa wa elimu umerejeshwa kama ulikuwa hapo awali ambapo mwanafunzi baada ya kumaliza Sekondari katika kidato cha nne alipata fursa ya kwenda kwenye vyuo vya ufundi kwa miaka 3 na kupata diploma ya fani husika iliyomwezesha kujiunga na masomo ya Chuo Kikuu.

Rais Samia yupo katika siku ya nne ya ziara ya kikazi mkoani Simiyu kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo na utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here