Chatanda apongeza utekelezaji wa Ilani ya CCM Kibaha

0

MWENYEKITI wa Umoja wa Wanawake Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (UWT-TAIFA), Mary Pius Chatanda, amefanya ziara ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM 2020/2025 katika miradi ya maendeleo ya jamii ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha.

Katika ziara hiyo, Chatanda ametembelea miradi ya sekta ya afya, elimu, maji, viwanda na ujenzi, ikiwemo Stendi ya Mlandizi inayojengwa kwa mapato ya ndani ya Halmashauri.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Shule ya Msingi Mtongani, amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mafanikio makubwa katika kusogeza huduma za kijamii karibu na wananchi kupitia sera ya “Kumtua Mama ndoo kichwani.”

Aidha, Chatanda ametoa pongezi kwa Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini na Mkurugenzi wa Halmashauri kwa usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo.

Pia, aliwaongoza wananchi na viongozi katika harambee ya kuchangia ujenzi wa nyumba ya mtumishi wa UWT eneo la Disunyara ambapo ahadi ya Shilingi Milioni 11.2 ilitolewa ili kukamilisha ujenzi huo.

Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Nickson John, alimueleza mgeni huyo mafanikio yaliyopatikana katika miaka mitano ya uongozi wa Rais Samia, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa shule mpya, vituo vya afya, na Hospitali ya Wilaya.

Aliongeza kuwa, Kibaha ni miongoni mwa maeneo yaliyonufaika na uwekezaji mkubwa kupitia kongani za viwanda za Modern Industrial Park na SINOTAN, pamoja na Bandari Kavu ya Kwala.

Chatanda amehitimisha ziara yake kwa kuwahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi katika Uchaguzi Mkuu ujao na kumchagua Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na viongozi wa CCM ili kuendeleza kasi ya maendeleo nchini.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here