Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
SERIKALI imeendelea kupongezwa kila kona kwa uwekezaji mkubwa uliofanya katika bandari mbalimbali hapa nchini hususani bandari ya Dar es Salaam kwa ufanisi mkubwa.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya ziara ya kikazi bandarini jijini Dar es salaam, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Dkt. Joseph Mhagama alisema, upanuzi na uboreshaji wa bandari hiyo imekuwa lulu kwa wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi.
“Leo tumekuja kwenye ziara yetu ya kawaida ya kikazi iliyo lengo la kujionea utekelezaji wa miradi ya uboreshaji na upanuzi wa bandari hii ya Dar es Salaam”, alisema Dkt Mhagama.
Dkt. Mhagama aliongeza kuwa, taarifa ya uwekezaji huo haipo kwenye makaratasi tu, bali ipo kwa vitendo, ndio maana mapato ya bandari yameongezeka na idadi ya wateja imeongezeka pia.
“Kwa hakika uwekezaji wa bandari hii ukioongezeka utafanya Bandari hii kuwa ni kitovu cha Utalii nchini, kwani mpaka hivi sasa kwenye mapato ya TRA yanaonesha bandari hii imechangia kwa asilimia 30”, alisisitiza Dkt Mhagama.
Aidha, Dkt Mhagama alisema kuwa wao kama kamati inayohusiana na masuala ya sheria mbalimbali, watashirikiana na TPA pamoja na Wizara ili kuhakikisha changamoto za kisheria zinatatuliwa ili kuongeza ufanisi kwa mamlaka hiyo kwani wameambiwa muingiliano wa kisheria ni mojawapo ya changamoto wanayokumbana nayo.
“Pamoja na hayo yote, kwa niaba ya Kamati hii ambayo mimi ninaiongoza tunampongeza Rais Samia kwa uthubutu na uwekezaji mkubwa anaoufanya kwenye miradi mbalimbali ya kimkakati sio tu hapa bali miradi yote hapa nchini,” alihitimisha Dkt. Mhagama.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile akimuwakilisha Waziri wa Wizara hiyo Profesa Makame Mbarawa alisema, wamepokea taarifa hiyo ya Kamati ya Bunge na kuahidi kuifanyia kazi.
“Nipende kuipongeza kamati hii, kwani mara zote imekuwa na maono kama aliyonayo Rais wetu Dkt Samia Suluhu Hassan ya kutaka bandari zetu ziwe zinachangia pato kubwa katika nchi,” alisema Kihenzile.
Aidha, Kihenzile alisema mipango ya Serikali ni mikubwa na ni endelevu ndiyo maana kamati imefurahi na kuipongeza Serikali kwa uwekezaji huo uliofanywa kwa bandari mbalimbali hasa ya Dar es Salaam, Tanga, Mtwara na nyinginezo za maziwa.
“Licha ya hayo Serikali inaendelea na ujenzi wa meli aktika ziwa Tanganyika na ziwa Viktoria, ambapo moja ya ziwa Viktoria ipo kwenye majaribio na muda siyo mrefu itaanza kazi”, alielezea Kihenzile.
Pamoja na hayo waziri Kihenzile alisema, miradi hiyo yote inayojengwa imelenga kurahisa biashara na kutoa huduma bora kwa wananchi na kuwapunguzia ugumu wa maisha wananchi hasa kwa kuwasogezea karibu huduma zote muhimu.
Naye, Mbunge wa viti maalumu kutoka mkoa wa Dar es Salaam wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Agnesta Kaizer alisema kuwa hana budi kumpongeza Rais Samia pamoja TPA kwa uwekezaji uliofanyika bandarini hapo na kufanya mazingira ya biashara yawe rahisi zaidi.
“Hii ni mara yangu ya kwanza kuja huku bandarini mara baada ya uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali pamoja na wawekezaji, nilikua nasikia taaarifa za maboresho ya bandari hii kwenye vyombo vya habari pekee, lakini leo nimeamini” alisema Kaizer.