NAIBU Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Khamis Hamza Khamis amesema si kila changamoto ni za Muungano, zipo zingine ambazo ni za kisekta zinazotakiwa kujadiliwa na kutatuliwa na sekta zenyewe.
Alisema, endapo sekta zimekutana na zikashindwa kufikia muafaka changamoto hizo zinawasilishwa katika Ofisi ya Makamu wa Rais inayosimamia Muungano ambapo wataalamu wanazijadili kisha makatibu wakuu, mawaziri na mwisho zinatatuliwa kupitia vikao vya Kamati ya Pamoja ya Serikali ya Jamhuri ya Muungani wa Tanzania (SJMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).
Naibu Waziri Khamis alisema hayo wakati akijibu maswali ya Mbunge wa Mwera Zahor Mohammed Haji bungeni jijini Dodoma leo Juni 6, 2025 aliyetaka kujua ni vigezo gani Serikali inaweka kutambua changamoto za Muungano.
“Ili iitwe changamoto ya Muungano na kuingizwa kwenye orodha ya hoja za Muungano ni lazima iwe na uzito na kujadiliwa kama nilivyosema awali ikija kwenu inapitia kwenye hatua mbalimbali na hatimaye kwenye Kamati ya Pamoja ya Serikali zote mbili chini ya uenyekiti wa Makamu wa Rais na Makamu wa Pili wa Rais,” alisema.
Aidha, Khamis alisema Serikali inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu hoja za Muungano zilizosalia kupitia vyombo vya habari, mitandao ya kijamii, makongamano, mijadala na vitabu vilivyoandaliwa na Ofisi ya Makamu wa Rais.
Kwa upande mwingine, alisisitiza kuwa Muungano ni wa nchi mbili, hivyo kuna umuhimu wa pande hizo kukaa pamoja na kujadili changamoto zinapojitokeza ndio maana huchukua muda mrefu kuzitatua.
Alisema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Kinondoni Tarimba Abbas aliyeuliza kama Serikali haioni haja ya kutatua haraka changamoto kwani ina uzoefu mkubwa hasa ukizingatia ni miaka 60 sasa tangu kuasisiwa kwa Muungano.
Awali, akijibu swali la msingi la Zahor, Naibu Waziri Khamis alisema taarifa ya utekelezaji wa ufumbuzi wa changamoto za Muungano inatarajiwa kutolewa kwa umma mara baada ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wake.
Alisema hayo wakati akijibu swali la mbunge kuhusu ni lini Serikali italeta muswada wa sheria kuhusu changamoto za Muungano zilizopatiwa ufumbuzi ili sasa ziwe kwa mujibu wa sheria.
Naibu Khamis alisema katika kikao cha Kamati ya Pamoja ya SJMT na SMZ kilichofanyika Aprili 4, 2025 Ikulu Dar es Salaam kwa ajili ya kutafuta ufumbuzi wa changamoto za Muungano kilitoa maelekezo kwa Ofisi za Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa SJMT na SMZ kufanyia kazi jambo hilo.