▪️Hatua hiyo kuongeza uzalishaji wa madini nchini
▪️Nyamongo kuanzishwa Kituo cha Elimu ya Uchenjuaji Madini
▪️Wachimbaji Wadogo wampongeza Rais Samia juu mafanikio sekta ya Madini
▪️Waziri Mavunde asisitiza juu ya uwezeshwaji Watanzania kimtaji
Musoma, MARA
SERIKALI kwa ushirikiano na sekta binafsi imejipanga kuanzisha vituo vya ukodishaji mitambo ya uchimbaji madini kwa wachimbaji wadogo ili kuwawezesha kutumia teknolojia za kisasa kufanya shughuli zao kwa tija.
Hayo yamesemwa leo, Juni 6, 2025 na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde wakati akihitimisha Kongamano la Maonesho ya Madini mkoani Mara kwenye viwanja vya Mukendo vilivyopo Manispaa ya Musoma.
“Sote tunatambua kwamba wachimbaji wadogo hawana uwezo wa kununua na kuihudumia mitambo ya kisasa kama kwa ajili ya uchimbaji.

Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametuelekeza Wizara ya Madini kuja na mpango huu ili kuwawezesha wachimbaji wadogo kupata fursa ya kutumia teknolojia ya kisasa kwenye shughuli zao lengo la kuongeza tija na uzalishaji wa madini.
Sambamba na Mitambo ya kukodisha tunatarajia pia kuanzisha Kituo cha Elimu ya Uchenjuaji wa madini ambacho kitakuwa na Mtambo wa Uchenjuaji wa madini eneo la Nyamongo-Tarime.

Ni matarajio yetu sasa kwamba mpango huu unakwenda kubadilisha uchumi wa wachimbaji wadogo kwa kuinua vipato vyao na hatimaye kuongeza mchango zaidi kwenye ukusanyaji wa maduhuli yatokanayo na sekta ya Madini,” alisema Mavunde.
Awali, akisoma taarifa ya sekta ya madini kwa Mkoa wa Mara, Mhandisi Amin Msuya alisema kuwa katika kipindi cha miaka minne ya Rais, Mkoa wa Mara umezalisha dhahabu tani 58.90 zenye thamani ya Shilingi Trilioni 6.90 kwa wachimbaji wadogo, kati na wakubwa.

Akitoa salamu za wachimbaji, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Madini Tanzania, John Wambura Bina amempongeza Rais Samia S. Hassan kwa kazi kubwa aliyoifanya kwenye sekta ya madini na kutoa rai kwa wachimbaji wadogo kuchangamkia fursa zilizopo Mkoani Mara na kuwahimiza kufuata Sheria na taratibu zilizowekwa kwani Serikali imeziboresha ili kulinda maslahi ya wachimbaji wadogo nchini.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi alieleza kwamba, lengo la kongamano hilo ni kuleta pamoja wadau wa sekta kujadili fursa zilizopo mkoani Mara na namna ya kuzifikia. Aidha, alisisitiza kuwa kongamano hili litaendelea kufanyika kila mwaka ili liwe chachu ya kuongeza mchango wa sekta ya madini kwenye GDP ya Mkoa ambao kwa sasa umefikia asilimia 18.
