NAIBU Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI anayeshughulikia afya Prof. Tumaini Nagu amesema Hali ya upatikanaji wa dawa Nchini katika ngazi ya afya Msingi ni ya kuridhisha tofauti na nyakati zilizopita.
Prof. Nagu ameyasema hayo wakati alipotembelea katika Hospitali ya Wilaya ya Chalinze mkoani Pwani katika ziara ya Usimamizi shirikikishi ya upatikanaji wa huduma za afya, Lishe na Ustawi wa Jamii.
“Tumeshuhudia katika kituo hiki upatikanaji wa dawa ni kwaasilimia kubwa na hii sio hapa pekee bali ni kwa vituo vyote hapa Nchini katika ngazi ya afya Msingi tupo Kwa wastani wa 85% ya upatikanaji wa dawa”.
Alisema, Hali imetokana na jitihada kubwa ambazo Serikali imekuwa ikifanya, ambapo Kila mwezi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa akitenga zaidi ya Bil. 16.6 kwaajili ya upatikanaji wa dawa.
Aidha, amevitaka vituo vyote vya kutolea huduma za afya ngazi ya afya Msingi kuhakikisha wanatunza dawa hizo vizuri.
Pia, amewataka wananchi kujiunga na mfuko wa bima ya afya Kwa wote ili kufanikisha upatikanaji wa huduma za afya kwa mtu yeyote na mahali popote pindi atakapopata changamoto za kiafya.