📌Mramba ashiriki Marathon ya Kuhamasisha Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia
📌 Asema Nishati Safi ya Kupikia itapunguza uharibifu wa mazingira na kulinda afya
KATIBU Mkuu wa Wizara Ya Nishati Felchesmi Mramba amesema, suala la upatikanaji wa nishati safi ya kupikia ni moja ya vipaumbele vya nchi na kwamba Serikali inahakikisha kuwa Mpango Mkakati wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia unatekelezwa kwa kasi na kwa umakini ili kutimiza azma ya nchi kuhama kutoka matumizi ya nishati isiyo safi ya kupikia kwenda kwenye nishati safi.
Alisema hayo Mei 17, 2025 jijini Dar es Salam wakati akishiriki Marathon ya Nishati Safi ya Kupikia iliyofanyika katika viwanja wa Oysterbay.
“Serikali imeamua kwenda nalo kasi suala hili la nishati safi ya kupikia ili kuepusha uharibifu wa mazingira kwani nishati ambayo si salama kama kuni na mkaa inatumika kwa kiasi kikubwa kwa kupikia hivyo tukitekeleza Dira hii, kwa kiasi kikubwa tutapunguza uharibifu wa mazingira pamoja na kulinda afya za wananchi.” alisema Mramba.
Mhandihi Mramba, amewapongeza waandaaji wa Marathon hiyo Shirika la Wafanyabishara Wanawake (TABWA) ambayo imelenga kuhamasisha Nishati Safi ya Kupikia kwa Wananchi.
Aidha, amewaasa Wadau mbalimbali kuzidi kujitokeza ila kuzidi kuendeleza mikakati ya kusambaza elimu ya Nishati Safi ya Kupikia kwa Watanzania wengi zaidi.