Serikali kutumia Bilioni 208.9 kuwezesha kaya duni kwa miaka sita

0

SERIKALI inakusudia kutumia Dola milioni 77.4 sawa na Shilingi Bilioni 208.9 kuzijengea uwezo kaya duni 260,000 (Laki mbili na elfu Sitini) za wakulima na wavuvi kwa kuziwezesha kitaalam na kifedha kwa muda wa miaka sita mfululizo ili ziweze kujiimarisha kiuchumi kupitia uzalishaji wa mazao ya uvuvi na kilimo.

Kaya hizo ambazo ni sawa na watanzania 1,300,000 (Milioni moja la laki Tatu) waliopo kwenye Mikoa 11 ya Tanzania Bara zinajengewa uwezo kupitia Programu ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP) katika mradi unaolenga kuimarisha Mifumo jumuishi ya usalama wa chakula na lishe kwenye Halmashauri 41 zinazounda Mikoa hiyo.

Ili kuwezesha utekelezaji chanya wa programu ya AFDP, Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge na Uratibu ambayo inaratibu programu hiyo kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI ambao ni watekelezaji imewakutanisha Makatibu Tawala wa Mikoa yote 11, pamoja na maafisa viungo kwenye halmashauri husika ili kujenga uelewa wa pamoja katika utekelezaji wa programu hiyo.

Akifungua kikao kazi hicho kinachoendelea mkoani Morogoro, Mkurugenzi wa Tawala za Mikoa Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Beatrice Kimoleta, amewasisitiza watendaji hao kusimamia kikamilifu pesa zote zitakazotolewa kwa lengo la kuwezesha utekelezaji wa mradi akikemea ubadilishwaji wa matumizi ya pesa za miradi.

“Hapa naomba nisisitize hizi pesa zisitumike kinyume na taratibu zilizoelekezwa katika utekelezaji wa programu hii, Serikali inahitaji kuona matokeo chanya kama yanavyolengwa na programu, isitokee mkabadilisha hata shilingi ya matumizi ya pesa hizi, kufanya hivyo itakuwa ni kama dhuluma kwa walengwa, na sitarajii mtu yeyote kubadilisha matumizi” alisema Kimoleta.

Awali, akitoa taarifa ya Programu hiyo Salimu Mwinjaka ambaye ni mratibu wa programu ya AFDP ameitaja mikoa itakayonufaika na programu hiyo kuwa ni Morogoro, Manyara, Singida, Dodoma, Tabora, Mwanza, Lindi, Pwani, Shinyanga, Geita na Tanga.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here