HALMASHAURI ya Wilaya ya Kibaha imetoa elimu ya usalama barabarani kwa madereva wa Serikali pamoja na watumishi wa umma katika Ukumbi Mkubwa wa Halmashauri hiyo, lengo likiwa ni kupunguza ajali zisizo za lazima barabarani.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Kamanda wa Polisi wa Usalama Barabarani wa Wilaya ya Kipolisi Mlandizi, ASP Rose John Mbaga, aliwasisitiza madereva na watumiaji wote wa vyombo vya moto kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepusha ajali.
“Mafunzo haya ni muhimu sana kwa watumiaji wa vyombo vya moto kwani huchangia kwa kiasi kikubwa katika kupunguza ajali zisizostahili. Ili kuepusha ajali, ni lazima madereva wazingatie kanuni za udereva wa kujihami,” alisema Kamanda Mbaga.
Awali, akifungua rasmi mafunzo hayo, Afisa Utumishi wa Wilaya, Edward Masona, aliwataka madereva wa serikali kuwa mfano bora kwa madereva wengine kwa kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani.
Kwa upande wao, madereva wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha wameahidi kutekeleza mafunzo hayo kwa vitendo, ili kusaidia kupunguza ajali zisizo za lazima katika maeneo mbalimbali ya barabara.