Na Mwandishi Wetu, Arusha
WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) ni miongoni mwa taasisi zilizoalikuwa kushiriki kutoa mada mbalimbali katika kikao kazi cha Makatibu wa Kamati za Bunge la JMT kinachoendelea katika Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki Jijini Arusha.
Katika wasilisho hilo, TFS ilieleza kuwa utalii ikolojia ni miongoni mwa nyanja zenye nafasi kubwa ya kukuza pato la taifa na kuongeza ajira, iwapo rasilimali za misitu na maeneo ya hifadhi zitasimamiwa ipasavyo.
Kauli hiyo ilitolewa leo, Ijumaa Agosti 29, 2025, na Mhifadhi Yusuph Tango kutoka Makao Makuu ya TFS jijini Dodoma, alipowasilisha mada kuhusu โUtalii Ikolojia na mafanikio yake TFSโ katika kikao kazi cha Makatibu wa Kamati za Kudumu za Kudumu za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kinachoendelea jijini Arusha kuanzia Agosti 25 hadi 31, 2025.
Tango alisema TFS imewekeza katika kuendeleza utalii ikolojia unaojikita katika misingi ya uhifadhi endelevu, elimu, ushirikishwaji wa jamii na uendelevu wa kiuchumi.
Alibainisha kuwa maeneo ya hifadhi za misitu yamekuwa yakivutia wageni wa ndani na nje ya nchi, huku miradi ya ushirikiano na jamii ikisaidia kuongeza kipato na kupunguza utegemezi wa misitu kama chanzo cha kuni na mkaa.
โUtalii ikolojia unajengwa juu ya kanuni kuu nne: uhifadhi, elimu, uzoefu wa kipekee na maendeleo ya jamii. Ndiyo maana tunasisitiza misitu yetu isiangaliwe tu kama vyanzo vya mbao au mazao ya misitu, bali pia kama nyenzo muhimu za kuvutia watalii na kukuza mapato ya serikali kutokana na huduma zitokazo na misitu,โ alisema Tango.
Mbali na mada hiyo, Mhifadhi Karim Solyambingu pia aliwasilisha taarifa kuhusu โHali ya Uhifadhi wa Misitu na Nyuki nchiniโ ambapo alieleza hatua zinazochukuliwa na serikali kupitia TFS kuhakikisha usimamizi wa rasilimali misitu na nyuki unakuwa endelevu licha ya changamoto za uvamizi, mabadiliko ya tabianchi na ongezeko la mahitaji ya rasilimali hiyo.
Kikao hicho cha makatibu wa Kamati za Kudumu za Bunge kinafanyika katika Ukumbi wa Bunge la Afrika Mashariki jijini Arusha, kikilenga kufanya tathmini ya utekelezaji wa majukumu ya kamati za Bunge la 12 lililomaliza mda wake.
Aidha, wizara na taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii zilipewa fursa ya kuwasilisha mada ili kuwajengea uelewa washiriki kuhusu utekelezaji wa shughuli zake.
Mbali na TFS, taasisi nyingine zilizoshiriki kutoa mada ni Mfuko wa Misitu Tanzania (TaFF) na Idara ya Wanyamapori (WD).